WAWILI WAHUKUMIWA KESI YA UBAKAJI PANGANI, AKIWEMO MVULANA WA MIAKA 10.

Mahakama ya wilaya ya Pangani, imemuhukumu  kifungo cha maisha gerezani  kijana ABDALLAH HAMISI mwenye umri wa miaka 19 baada ya kupatikana na hatia ya kumbaka binti mwenye umri wa miaka 6 ambae ni mwanafunzi wa darasa la kwanza. (Taarifa zake tumedhihifadhi kwa sababu za kimaadili)

Katika kesi hiyo ya jinai namba 14 ya mwaka 2019,iliyokuwa na watuhumiwa wawili ambapo ilidaiwa katika hati ya mashtaka iliyowasilishwa na polisi mahakamani hapo, kuwa mnamo  tarehe 13/03/2019 ndani ya wilaya ya Pangani washtakiwa hao walimbaka binti huyo huku wakijua kuwa ni kosa kisheria.

Awali watuhumiwa hao walishitakiwa kwa makosa mawili ambayo ni kubaka na kulawiti ila baadae mahakama iliwatia hatiani na kosa la kubaka.

Mtuhumiwa wa kwanza aliyefahamika kwa jina la Abdallah Hamisi mwenye umri wa miaka 19 ameukumiwa kifungo hicho cha maisha,na mwengine mvulana mwenye umri wa miaka 10 ambapo  kutokana na umri wake alihukumiwa kifungo cha nje kwa muda wamiezi 12 na  kutakiwa kutokutenda kosa  lolote  kwa kipindi hicho.

Hukumu hiyo imetolewa tarehe 29 ya mwezi wa 4 mwaka huu 2020 katika Mahakam ya wilaya Pangani mbele Hakimu mkazi mfawidhi mahakama ya wilaya ya Mheshimiwa JOEL MNGUTO.