MTOTO WA MIAKA MIWILI APOTEZA MAISHA BAADA YA KUTUMBUKIA KISIMANI.

Mtoto mmoja anayekadiriwa kuwa na umri wa miaka miwili mkazi wa kitongoji  cha Uhindini  mjini Pangani Mkoani Tanga amethibitishwa kufariki dunia hapo juzi jumamosi baada ya kutumbukia katika kisima chenye maji.

Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo mkuu wa kituo cha POLISI PANGANI Mrakibu Msaidizi wa Polisi PAULO ISUJA  amesema tukio hilo limetokea Jummosi wakati mtoto huyo akicheza na wenzake na kwamba mwili wa mtoto huyo tayari umekwishazikwa na ndugu zake.

“ tukio hilo limetokea Pangani maeneo ya uhindini ni tukio lililosikitisha watu wengi, kwa maelezo tuliyopata ya awali mtoto huyo alikuwa akicheza na wenzake baadae akaonekana ametumbukia kweny kisima.” Amesema Bwana Paulo Isuja.

Aidha bwana Isuja amesisitiza wazazi kuwa makini na kuchukua tahadhari katika kulinda watoto wao dhidi ya ajali kama hizo kwa kufunika visima vyao.

“Wazazi walezi na kila mmoja wetu anawajibika kulea tuwe makini sana na watoto wanapokuwa wanacheza wale wote wanaomiliki visima au hata kiwe cha aina gani tafadhali, watu wajitahidi kuvifunika visima hivyo pale tu inapobidi mtu anataka kuchukua maji ndiyo vifunguliwe lakini tukiacha wazi mtoto anaweza kutumbukia kwahiyo matukio hayo yapo.” Ameongeza Bwana Isuja.

Katika hatua nyingine Bwana Isuja amewataka wananchi kufukia mashimo yaliyokaribu na makazi ya watu yanayoweza kujaa maji kwa kipindi hiki cha mvua na kupelekea maafa.

Ulinzi na usalama kwa mtoto ni miongoni mwa haki muhimu kwa mtoto kwakuwa mtoto anastahili kulindwa katika maeneo mbalimbali ikiwemo nyumbani na hata shuleni  huku wazazi na walezi wakiwa ndiyo wenye jukumu kubwa kiutekelezaji.