SOMA HII KABLA HUJAENDA KWA MGANGA WA TIBA ASILI PANGANI.

Waganga wa Tiba za Asili na Tiba Mbadala Wilayani Pangani Mkoani Tanga wametakiwa kuzingatia Maagizo ya Serikali na Maelekezo ya wataalam wa Afya yanayotolewa, ili kujilinda na Maambukizi ya Virusi vya Corona wao na wateja wanaofuata huduma zao.

Akizungumza na Pangani fm kwa njia ya simu Katibu wa Waganga wa Tiba za Asili na Tiba Mbadala Wilayani Pangani kupitia chama cha UWAMATA Taifa, Bwana Rashidi abdallah amesema kwa waganga waliosajiliwa na kutambulika waongeze umakini katika utoaji wa huduma zao ili kuepusha kusambaa zaidi kwa virusi vya Corona.

“Ninachowasihi waganga waliosajiliwa wawe makini na haya maradhi kwani yanaua, wahakikishe wateja wao wanafuata maelekezo ya wataalam wa afya wanapofuata huduma ili kujikinga na maradhi haya waache ubishi”.

Aidha, mbali na kuwataka waganga kufanya kazi zao katika mazingira safi, pia amewaonya waganga wanaofanya kazi bila kusajiliwa akisema ndio ndio chanzo cha Uvunjaji wa Taratibu zinazoelekezwa na Serikali.

“Kama Katibu wa Waganga Pangani na mtafiti wa Waganga natoa onyo kwa waganga wote ambao hawajasajiliwa tutawachukulia hatua kwa sababu ndio chanzo kikubwa cha maradhi kutokana na kuagua bila kufuata sheria”. Na kuongeza kuwa…. “Kabla ya Maradhi haya nilikuwa Dar es Salaam nikazungumza na viongozi wakuu wakasema watakuja Pangani na kutembelea nyumba ya mganga hadi mganga tutakayemkuta hajasajiliwa tutamchukulia hatua na alosajiliwa tujue anatoa tiba kivipi maana sisi waganga wenyewe kuna wengine vilinge vyao vichafu na maradhi yanatokana na Uchafu”.

Hata hivyo Katibu huyo wa Waganga wa Tiba za Asili Pangani, ameelezea namna shughuli zake zilivyoathirika kutokana na janga la Corona kutokana na wateja wanaofuata huduma zake kupungua kutoka ndani na nje ya Tanzania, ambao amelazimika kuwasimamisha kuja kama hatua za kujihadhari na Corona.

“Tangu yalipoingia haya Maradhi kwanza wateja hakuna kama huko nyumba, lakini bado mimi mwenyewe nimewasimamisha wateja wangu wengi tu Ndani na Nje ya Nchi, na nimeamua kuwasimamisha ili kuepusha mikusanyiko ya watu kwani inawezekana ikawa ndio chanzo cha kuambukizana. Kwa hiyo mie nimewasimamisha wateja wangu wengi kutoka nje ya Tanzania kama Kenya, Congo, Uarabuni, Afrika Kusini”.

Maeneo ya Waganga wa tiba za asili na tiba mbadala ni miongoni mwa sehemu zinazopokea watu wengi kutoka kona mbalimbali ulimwenguni ambao hufuata huduma kutokana na matatizo waliyonayo, hivyo basi wakati serikali kupitia wataalam wa afya wakiendelea kutoa elimu ya kujikinga dhidi ya virusi vya Corona, hali imekuwa hivyo pia kwa waganga wa tiba asilia Wilayani Pangani ambao nao wamekuwa mstari wa mbele kuhakikisha wanajikinga kabla ya kutoa tiba kwa wagonjwa wao na kulazimika kuwasimamisha wengine hasa kutokana na kuongezeka kwa idadi ya maambukizi ya ndani kwa ndani nchini.