KUELEKEA EID AL-FITR 2020 PANGANI MASHARIKI WAJIPANGA DHIDI YA CORONA.

Uongozi wa Kijiji cha Pangani Mashariki Wilayani Pangani Mkoani Tanga umeahidi kuendelea kushirikiana na Jeshi la Polisi kipindi chote cha Sikukuu, ili kuzuia Mikusanyiko iliyokuwa ya lazima kama tahadhari ya kuendelea kukabiliana na Janga la Corona.

Akizungumza na Kituo hiki Mwenyekiti wa Kijiji cha Pangani Mashariki Bwana Rajabu Kitwana Nyembo, amesema kuwa ni vyema Mwaka huu Familia kwa pamoja zikafurahia Sikukuu ya Eid el Fitri Nyumbani kwa utulivu, huku wakizingatia maelekezo ya Serikali na Wataalam wa Afya dhidi ya Corona.

“Sisi hatutarudi nyuma katika kushirikiana na Jeshi la Polisi hasa kwa kipindi hiki, kwa hiyo nazisihi familia sisi tunachotaka ni utulivu bado Corona ipo, kwa hiyo ni vyema siku ya Eid el Fitri familia zikasherehekea sikukuu kwa pamoja nyumbani huku wakiendelea kuzingatia tahadhari zote zilizotolewa, na sisi tutalisimamia hili”. Amesema Mwenyekiti wa Kijiji hicho.

Aidha Bwana Nyembo mbali na kutoa maelekezo kwa wamiliki wa kumbi za Starehe ndani ya kijiji hicho, pia ametuma salamu kwa Wananchi walio Nje ya Pangani ambao wanampango wa kutembelea Wilayani humo kwaajili ya kufurahia Mazingira.

“Sisi katika kijiji chetu tumebarikiwa Bahari inayopendeza na kuvutia machoni mwa wengi na ndio maana siku kama hizi za Sikukuu tunapata wageni kutoka maeneo mbalimbali wanakufa kufurahia mazingira mazuri huku wenyeji nao wakinufaika kwa kuwa biashara na bidhaa zao zinanunuliwa.” Na kuongeza kuwa…

 “Lakini kutokana na wakati huu tulio nao wa Janga la Corona Mwaka huu itakuwa tofauti, hatuta ruhusu Picnic maeneo ya ufukweni na pia hatuta ruhusu kwenye kumbi za Starehe wafanye kama wanavyofanya miaka ya nyuma, wafahamu haturuhusu ili kujikinga na Corona.”

Eid al-Fitr ni Siku kuu inayosherehekewa na Waumini wa Dini ya Kiislamu Ulimwenguni kote baada ya kumalizika kwa Mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhan, na Mwaka huu Siku kuu hiyo itasherekewa kwa tahadhari kubwa Duniani kote kutokana na kwamba Ulimwengu bado unakabiliwa na Janga la Corona .