ULINZI SHIRIKISHI KATIKA VIJIJI 33 VYA PANGANI.

Ili kuendelea kudhibiti Vitendo vya uhalifu kwenye Jamii Wilayani Pangani Mkoani Tanga, Vijiji vyote 33 vilivyopo Wilayani humo, vimetakiwa kuanzisha na kusimamia Vikundi vya Ulinzi Shirikishi na kuhakikisha vinakuwa endelevu ili kubaini na kudhibiti Matukio hayo kwenye Maeneo yao.

Hayo yamesemwa na Mratibu wa Polisi Jamii Wilayani humo Inspekta Haruna Hassan wakati akizungumza na kituo hiki ambapo amesema kuwa uanzishwaji wa Polisi Jamii ni takwa la kisheria hivyo Vijiji vinapaswa kulitekeleza.

Meneo yote kwa maana ya Kata na Vijiji kuanzishwe vikundi vya ulinzi shirikishi, haya ni matakwa ya kisheria katika katiba ya uchaguzi ilani ya uchaguzi 2015/20 ibara ya 146 (5), sheria za halmashauri za wilaya namba 7 na 8, sheria ndogondogo za vijiji zote hizo zinaelekeza uanzishwaji wa vikundi vya ulinzi shirikishi ikiwemo sungusungu.

Kwa hiyo nivitake tu vijiji na kata husika vianzishe vikundi hivi vitasaidia sana katika kutatua kero za uhalifu.  – Amesema Inspekta Haruna  Hassan

Hata hivyo baadhi ya Vijiji tayari wameshalitekeleza suala hilo ikiwemo Kijiji cha Pangani Magharibi, ambapo Kijana Nasib Saidi anayejitolea kama Polisi Jamii, anaeleza baadhi ya changamoto zinazowakabili wakati wanapokuwa doria.

β€œUnaweza ukakutana na watu ukawasimamisha ukawauliza na wao wanakuuliza wewe ni nani kwa hiyo hilo jambo linatutatiza kidogo, unaweza kumwambia mimi ni Fulani nipo kwa ajili ya suala Fulani mtu anakuzarau. Kwa hiyo tunawaomba viongozi mtusaidie katika suala hili hata kwa kutupatia vitambulisho au sare kwa ajili ya sungusungu.- Polisi Jamii Pangani.”

Je Inspekta Haruna ambaye ndiye Mratibu wa Polisi Jamii Pangani, anazungumziaje hoja hiyo?

β€œHiki kikundi cha ulinzi shirikishi kisiwe ni kikundi cha mtu kiwe ni kikundi cha wananchi wenyewe, kwa hiyo baada ya kuteuliwa kwa sifa walizonazo lazima wapelekwe nyenye mkutano mkuu wa kijiji ili wanakijiji waweze kuwatambua, lakini la pili kuhusu uwepo wa kitambulisho au sare maalum sio mbaya ila itategemea uwezo wa kiuchumi wa eneo husika”.

Kwa upande wake Bwana Halfani Rashid Joho ambaye ni Afisa Mtendaji wa Kijiji cha Pangani Magharibi anasemaje kuhusu suala hili?

β€œHilo suala la vitambulisho tumelipokea kama halmashauri ya kijiji na tunataka kutenga bajeti kwa maana ya kuwatengenezea vitambulisho, nafikiri baada ya wiki mbili itakuwa tumeshalimaliza hili tatizo”. Amesema Bwana Joho

Naye Mwenyekiti wa SunguSungu Pangani Magharibi Bwana Ramadhan Yona maarufu Sorinyo, amesema β€œushauri wangu kwa vijana wenzangu, watoke tushirikiane ili tuongeze nguvu, tujitoe pangani ni yetu wote pangani bila uhalifu inawezekana.”

Kushirikiana na kusaidiana kwa jamii inaweza kusaidia kudhibiti uhalifu na kupunguza hofu. Madhumuni ya vikundi hivyo ni kushirikiana na Jeshi la Polisi ili kutokomeza vitendo vya uhalifu.  Polisi jamii ilianzishwa rasmi nchini Tanzania mnamo 2006 kama sehemu ya mpango unaoendelea wa mageuzi ya polisi. Mbali na kujaribu kuboresha mawasiliano kati ya polisi na umma.