Radio yangu, Darasa Langu

4
Binti  Husna Omari ni mkazi wa kijiji cha Boza Wilayani Pangani Mkoani Tanga.  

Akizungumza huku akiwa anarekebisha Antena ya Redio ndogo ya kuchaji kwenye Umeme aliyopewa na Mama yake, huku  akiwa ameketi kwenye Mkeka na ameweka Redio hiyo pamoja na daftari lake jipya alilonununuliwa  maalum kwa ajili ya kujifunzia kupitia matangazo ya Redio Binti Husna anaelezea jinsi ilivyokuwa wakati amesikia tangazo la uwepo wa kipindi kitakachotoa nafasi ya wanafunzi kujifunza kupitia Redio  “Nilifurahi nikamwambia Bibi itakua tunasoma kwenye Redio sasa hivi…Bibi akaniambia tumshukuru Mungu”.

Husna ni binti wa miaka 13 ambaye ni mwanafunzi wa Darasa la saba katika shule ya msingi Boza iliyopo wilayani Pangani, mkoani Tanga.

Yeye ni mmoja wa maelfu ya wanafunzi wa shule za awali, msingi na Sekondari nchini Tanzania ambao wamelazimika  kusimama masomo tangu Machi 17 mpaka Juni 19 Mwaka 2020 kutokana na Serikali  kuzifunga Shule na Vyuo ili kuchukua tahadhari dhidi ya kuenea kwa maambukizi ya virusi vya Corona.  

Husna anaishi na Mama yake Bi. Jamila Abdallah pamoja na Bibi yake ambao kwa pamoja wameamua kubeba Majukumu ya kufanya baadhi ya shughuli za Nyumbani ambazo angetakiwa kuzifanya akiwa nyumbani ili kumpa nafasi ya kutulia kusikiliza na kujifunza kupitia kipindi maalum cha  Redio Pangani FM kilichopewa jina ‘Redio Darasa’.

Pamoja na hayo Mama yake amekuwa akimuwezesha kupiga Simu Studio kuuliza na kujibu maswali ya Waalimu.

Lengo la kipindi hicho ni kuwawezesha wanafunzi wa shule za Msingi na Sekondari ambao wamelazimika kubaki nyumbani kutokana na Janga la virusi vya Corona kuweza kujifunza kupitia Redio.


Baadhi ya Walimu wakiwa katika Kipindi ndani ya Studio ya Kurushia Matangazo ya Redio Pangani.

Kupitia kipindi hicho wanafunzi pia wanapata nafasi ya kuuliza maswali kwa walimu moja kwa moja kwa njia ya simu.

Walimu toka shule za Msingi na Sekondari zilizopo wilayani Pangani Mkoani Tanga ndio wanaoendesha kipindi hicho kwa kuwepo Studio ili kutoa nafasi kwa wanafunzi kuuliza maswali na kueleweshwa zaidi.

C60A0681
Husna anasema ndoto yake ni kuja kuwa Mwalimu na anaichukulia Redio Darasa kama yuko Darasani kwani anaelewa.