JESHI LA POLISI PANGANI LAHIMIZA AMANI KUELEKEA UCHAGUZI 2020

Jeshi la Polisi Wilayani Pangani Mkoani Tanga, limesema litahakikisha linawashughulikia wale wote watakaovuruga amani kipindi hiki cha Uchaguzi.
Hayo yamesemwa na Mratibu wa Dawati la Uchaguzi Pangani Inspekta Haruna Mohammedi, wakati akizungumza na Kituo hiki ambapo amesema kitakwimu Pangani iko salama, hivyo uchaguzi isiwe chanzo cha kuivuruga amani iliyopo.
Aidha Inspekta Haruna amesema kuwa wao kama Jeshi la Polisi wanao wajibu wa kulinda amani na usalama wa raia na mali zao, na kwamba litahakaikisha linawashughulikia wote wasiopenda amani.

Mbali na hayo Mratibu huyo wa Dawati la Uchaguzi Pangani amesema Jeshi la Polisi halitaweza kuwavumilia wagombea watakaonadi chuki, na kutoa lugha za kuudhi, huku akiwatahadharisha vijana kutokubali kuiharibu kesho yao kwa kutumika kisiasa na kushiriki maandamano ambayo yapo kinyume cha sharia.

Kwa upande wake Mkaguzi Msaidizi kutoka Ofisi ya upelelezi Wilayani Pangani Ramadhan Semjaila amesema uchaguzi ni kipindi kifupi na cha mpito kwenye maisha hivyo ameshauri wadau wote wa kisiasa kuzingatia sheria ili kuhakikisha amani na utulivu unakuwepo.

Madawati ya Uchaguzi yameanzishwa na yanapatikana Nchi nzima na yameanzishwa mahususi kwa ajili ya kufuatilia na kuratibu mambo mbalimbali yanayohusiana na uchaguzi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *