TAKUKURU PANGANI YAMUOKOA MWALIMU MSTAAFU NA KUMREJESHEA FEDHA TOKA KWENYE ‘MKOPO UMIZA’ WA RIBA YA 300%

Taasisi ya Kuzuia na kupambana na Rushwa TAKUKURU Wilayani Pangani Mkoani Tanga imefanikiwa kurejesha kiasi cha Fedha shilingi milioni nne na Laki Nne (4,400,000/= ) kwa bwana Hatibu Fue Mkanza ambaye ni Mwalimu mstaafu, fedha alizokuwa ametoa kama riba ya Mkopo.

Mnamo tarehe 05/05/2020 Ofisi ya TAKUKURU (W) Pangani ilipokea malalamiko toka kwa Mwalimu mstaafu Hatibu Fue Mkanza akimlalamikia mkopeshaji binafsi ndugu Maboga Juma Hitira kuwa mnamo mwaka 2017 alimkopesha fedha kiasi cha Shilingi 4,000,000 (Milioni Nne) kwa makubaliano kuwa atamrejeshea fedha hizo baada ya kulipwa mafao yake ya kustaafu na kwamba katika makubaliano yao riba ya mkopo haikuwekwa bayana kwa Mkopaji.

Ilidaiwa katika taarifa ya malalamiko kwamba mafao ya mstaafu huyo yalipotokea tarehe 11/10/2018 mkopeshaji huyo alimtaka amlipe jumla ya shilingi 16,000,000/= fedha ambayo ni Shilingi 12,000,000/= (Milioni Kumi na Mbili) zaidi ya kile alichopokea kutoka kwa mkopeshaji.

ilidaiwa na mlalamikaji kwamba kutokana na mazingira yaliyokuwepo na jinsi mkopeshaji alivyombana hadi kufikia tarehe ya kuwasilisha malalamiko yake TAKUKURU tayari mkopeshaji alishachukua toka kwake jumla ya Shilingi 8,400,000/= fedha ambazo alimlipa kupitia mafao yake ya kustaafu na kupitia ‘pension’ yake ya kila Mwezi.

Taarifa ilieleza kwamba pamoja na Mkopeshaji huyo kuchukua fedha hiyo bado anaendelea kumhujumu kwa kumtaka aendelee kumlipa hadi ifike 16,000,000 bila ya uhalali wowote.

Baada ya mtoa taarifa kubaini kuwa alidhulumiwa na mkopeshaji huyo na kwamba baada ya kuona na kusikia kupitia Vyombo vya Habari kwamba baadhi ya wastaafu wamekuwa wakirejeshewa fedha zao kwa msaada wa Takukuru ,ndipo aliamua kufika TAKUKURU Wilaya ya Pangani ili aweze kupata Haki yake.