WANANCHI PANGANI WAASWA KUJIUNGA NA BIMA YA CHF

Wananchi wilayani Pangani mkoani Tanga wameaswa kuwa na mwamko wa kujiunga  na bima ya afya ya jamii yaani CHF iliyoboreshwa ili kuwa na uhakika wa upatikanaji wa matibabu bora. 

Hayo yamezungumzwa na Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya wilaya ya Pangani ndugu HASSAN MSAFIRI katika kipindi cha Asubuhi ya leo kinachorushwa na kituo hiki, ambapo amesema kuwa Bima za Afya humsaidia mwananchi kupata matibabu yaliyo bora na kuepusha misamaha mingi ya matibabu kwa wagonjwa.

“Kama hautojiunga na mfuko wa CHF na wewe haupo hata katika bima ya taifa basi lazima utatuchangia katika huduma zetu, ili na sisi tuweze kujiendesha lakini tukisema tutoe misamaha mwisho wa siku tutashindwa kujiendesha kwahiyo nawashauri wananchi wenye uwezo basi wajiunge na bima za afya.” Amesema Dr. Hassan Msafiri.

Aidha Dkt. Msafiri amewasihi wananchi wote wa pangani kutoa ushirikiano na wataalamu wa afya katika kutoa taarifa muhimu zitakazosaidia kuboresha utoaji wa huduma za afya hospitalini hapo.

‘Napenda kutoa wito kwa wana pangani waonyeshe ushirikiano kwakuwa sisi ni binadamu kuna sehemu tunakosea na kuna sehemu tunapatia kwahiyo pale unapoona tumekosea basi ule utaratibu sahihi wa kupeleka yale malalamiko yako ufuatwe ili tutakapoyafanyia kazi yale malalamiko ndipo tunakuwa tumeboresha huduma zetu za afya.” Ameongezea Dr. Hassan Msafiri.

Bima ya afya ya Jamii yaani CHF iliyoboreshwa ni Bima inayogharimu kiasi cha shilingi Elfu 30 kwa watu Sita kwa Mwaka huku ikimuwezesha mgonjwa kutibiwa hadi katika Hospitali za Mkoa kwa mfumo wa rufaa.

Hayo yamejiri leo katika kipindi cha Asubuhi ya Leo wakati wa mahoajiano maalumu na Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Wilaya ya Pangani alipokuwa akitoa taarifa ya upokeaji wa vifaa mbalimbali vya Hospitali vilivyotolewa na  wazawa wa Pangani, watanzania na wadau mbalimbali wanaoishi nchini Ujerumani ili kusaidia utoaji wa huduma bora kwa Wananchi.