KISA WIVU WA MAPENZI AMSHAMBULIA VIBAYA MKE MWENYE MTOTO MCHANGA WA SIKU 21

Jeshi la Polisi Wilayani Pangani Mkoani Tanga linamshikilia Mwanaume mmoja kwa tuhma za kumjeruhi mke wake anayefahamika kwa jina la Tabia Omari sehemu mbalimbali za mwili wake kutokana na wivu wa mapenzi.

Akizungumza na Kituo hiki mapema leo Mkuu wa Upelelezi Wilayani Pangani ELIJA MATIKU amesema kuwa Mwanaume huyo amemjeruhi mke wake baada ya kuona wivu pale alipokwenda kumjulia hali mkewe Hospitalini na kumkuta akitoka chumba kimoja huku akiwa ameongozana na Mwanaume ambaye ni Muhudumu wa Afya.

“Huyu Mwanaume alifika Hospitali yetu ya Wilaya, baada ya kufika pale alimkuta mkewe akitokea chumbani akiwa ameambatana na Muhudumu mmoja wa afya wa kiume akaingiwa na wivu wa mapenzi akihisi labda mkewe ametoka kumsaliti lakini alijituliza, ila waliporudi nyumbani mume ndo akawa anakumbushia kitendo kile cha Hospitali mara kwa mara kukatokea mabishano na ugomvi hadi kufikia hatua ya mume kumjeruhi mkewe kichwani na sehemu mbalimbali za mwili wake”. Amesema Bwana Elija Matuku.

“Mwanamke aliyejeruhiwa ambaye anaitwa ametoka kujifungua na kwa sasa ana mtoto mdogo wa siku 21.” Amesema Mkuu huyo wa Upelelezi Pangani.

Aidha Bwana Matiku amesema kuwa pamoja na kumshikilia Mtuhumiwa wa tukio hilo, bado taratibu za upelelezi zinaendelea na ukikamilika watamfikisha Mahakamani kwa hatua Zaidi za Kisheria.

Matiku amemalizia kwa kutoa wito wake kwa wenza kuachana na wivu unaopelekea kufanyiana vitendo vya ukatili, huku akisema kitendo cha kujichukulia sheria mkononi ni kosa kisheria.